November 5, 2008

Obama rais mteule wa Marekani


BBC News (source)
Imeandikwa na Hassan Mhelela, Washington DC.

Barack Obama, mgombea kupitia chama cha Democrat, amechaguliwa kuwa rais mteule wa Marekani, akiwa ni mweusi wa kwanza katika historia ya taifa hilo kubwa duniani.Kwa mujibu wa matokeo ya awali.

"Imekuwa ni subira ya muda mrefu, lakini leo... mabadiliko yameishukia Marekani," rais huyo mteule aliueleza umati wa watu uliokuwa ukimshangilia katika viwanja vya Grant mjini Chicago.

Mpinzani wake, Bw John McCain alikubali kushindwa kwa kusema: "Ninamhusudu sana Bw Obama". Akatoa wito kwa wafuasi wake kuonyesha nia njema kwa rais mpya.

Kwa hakika matokeo hayo ya uchaguzi yatakuwa na mrindimo mzito kwa siasa za Marekani.

Anakadiriwa kuwa ameshinda kura za kutosha kumhakikishia ushindi wa kumbwaga hasimu wake John McCain wa chama cha Republican.

Wakati wa kuandika taarifa hii Bw Obama amepata kura 338 kati ya 538, za wajumbe wa kumchagua rais - electoral voters.John McCain alikuwa na kura 159.

Bw Obama alifika katika uwanja wa Grant akiwa na mgombea mwenza Joe Biden, kutoa hotuba yenye uzito wa kipekee.

"Endapo kuna yoyote hapa ambaye bado ana mashaka kwamba Marekani si mahali kwenye kutoa fursa kwa kila jambo, ambaye bado anajiuliza endapo ndoto ya wahenga wetu bado inaendelea katika kizazi chetu, ambaye bado anahoji nguvu ya demokrasia yetu, usiku wa leo ndilo jibu kwako," Bw Obama alieleza.

Alieleza kuwa amepigiwa simu muhimu kutoka kwa Bw McCain.Akamsifu mkongwe huyo wa vita vya Vietnam, "kuwa kiongozi jasiri na asiye mbinafsi".

Ushindi mzito


Bw Obama akiwa na familia yake baada ya hotuba ya kuitikia ushindi.
Bw Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani
Bw Obama alikwapua majimbo muhimu ya Pennsylvania na Ohio, kabla ya kufikisha idadi ya kura 270 za wajumbe wanaotakiwa kumpa rais ushindi kwa mujibu wa mfumo wa 'electoral college', kisha zikaja taarifa kuwa pia ameshinda California na mengine kadhaa.

Halafu zikafuatia habari kwamba ameshinda Florida, Virginia na Colorado - katika uchaguzi wa mwaka 2004 yote yalimpigia kura mgombea wa chama cha Republican - sasa ameyabadilisha kuwa majimbo ya Democrat.

Hata hivyo inaonyesha hakuna tofauti kubwa kati ya wagombea hao katika kura zilizopigwa na wananchi, wakiwa wameachana kwa asilimia chache.

Licha ya kushinda kiti cha rais, chama cha Democrat kimeongeza uwingi wa viti katika baraza la Congress.
Another blogger announces the news

0 comments:

  © Blogger templates The Professional Template by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP